21 Desemba 2025 - 12:54
Balozi Matinyi Auvunja Msimamo wa Kibeberu: Tanzania Si Taifa la Huruma, Bali Nguvu Inayoinuka Kiuchumi

Katika ujumbe wake mzito kwa jumuiya ya kimataifa, Balozi Matinyi alisisitiza kuwa Tanzania ya sasa inatafuta wafanyabiashara na wawekezaji, si wafadhili. Taifa linaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), pamoja na mradi wa gesi asilia unaokadiriwa kugharimu dola bilioni 42, miradi inayolenga kuimarisha uchumi wa taifa na nafasi yake katika uchumi wa kikanda na kimataifa.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Kwa miongo mingi, baadhi ya mataifa ya Magharibi yameendelea kuangalia Tanzania kupitia lenzi ya zamani ya kikoloni, yakiitaja kama nchi inayohitaji huruma na misaada ya kudumu. Taswira hiyo ya kupotosha ilijitokeza upya hivi karibuni pale Waziri wa Sweden, Benjamin Dousa, alipoitoa kauli kwamba Tanzania “imekwama kwenye Ujamaa” na “haina maendeleo.” Hata hivyo, kauli hiyo ilipokelewa kwa majibu mazito, yenye hoja na takwimu, kutoka kwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi.
Kupitia gazeti la Sweden Aftonbladet, Balozi Matinyi aliweka wazi kuwa Tanzania ya leo si ile ya mwaka 1961, wala si taifa linaloishi kwa kutegemea msaada wa wahisani wa nje. Badala ya kujibu kwa jazba, Balozi huyo alichagua njia ya hekima, akitumia takwimu halisi na mafanikio yanayoonekana kuonesha mabadiliko makubwa ya Tanzania katika sekta mbalimbali.
Balozi Matinyi aliwakumbusha Waswidi kuwa, wakati Sweden ikiwa na vyuo vikuu 18, Tanzania kwa sasa ina zaidi ya vyuo vikuu 36, hatua inayoonesha uwekezaji mkubwa katika elimu ya juu na rasilimali watu. Aidha, alifafanua kuwa dhana ya Tanzania kusubiri msaada wa Sweden wa takribani SEK milioni 560 (sawa na dola milioni 60) ni potofu, ikizingatiwa kuwa taifa hilo linakusanya zaidi ya dola bilioni 4 kila mwaka kupitia sekta ya dhahabu pekee.
Katika ujumbe wake mzito kwa jumuiya ya kimataifa, Balozi Matinyi alisisitiza kuwa Tanzania ya sasa inatafuta wafanyabiashara na wawekezaji, si wafadhili. Taifa linaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), pamoja na mradi wa gesi asilia unaokadiriwa kugharimu dola bilioni 42, miradi inayolenga kuimarisha uchumi wa taifa na nafasi yake katika uchumi wa kikanda na kimataifa.
Aidha, alibainisha kuwa uchumi wa Tanzania unaendelea kukua kwa kasi inayozidi ile ya baadhi ya mataifa ya Ulaya, jambo linalothibitisha kuwa nchi ipo katika mwelekeo sahihi wa maendeleo endelevu na uhuru wa kiuchumi.


Jibu la Balozi Matinyi halikuwa tu utetezi wa hadhi ya Tanzania katika ulingo wa kidiplomasia, bali lilikuwa ni tamko la wazi la uhuru wa kiuchumi na kujiamini kwa taifa. Kauli yake kwamba kuitaja Tanzania kama nchi isiyo na maendeleo ni “upotoshaji wa kusikitisha” imegusa hisia za Watanzania wengi na kuamsha fahari ya kitaifa.
Ni wakati muafaka kwa Watanzania kutambua na kujivunia hatua kubwa zilizopigwa. Tanzania imebadilika, imeimarika na inaendelea kupaa. Wanaodhani bado tupo gizani ni wale waliolala usingizi wa historia, wakati taifa likisonga mbele kuelekea mustakabali wa maendeleo, heshima na uhuru kamili wa kiuchumi.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha